Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) umepungua kwa Shilingi Bilioni 380 kutoka Shilingi Trilioni 20.2 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 19.9 kwa wiki iliyoishia Mei 19 mwaka huu.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa biashara katika soko hilo kwa kipindi cha wiki moja iliyopita kipindi ambacho mtaji wa kampuni za ndani nao ukiwa umepungua kwa Shilingi Bilioni 150 kutoka Shilingi Trilioni 7.21 wiki iliyopita hadi Shilingi Trilioni 7.06 wiki hii.

Aidha katika kipindi hicho, mauzo ya hati fungani yameongezeka kutoka mauzo yenye thamani ya Shilingi bilioni 22.6 hadi Shilingi bilioni 29.5; hii ikiwa ni kutokana na mauzo ya hati fungani tisa za serikali na hati fungani moja ya EXIM zenye jumla ya thamani ya Shilingi bilioni 39.5 kwa jumla ya gharama ya Shilingi bilioni 29.5.