Jumamosi , 18th Mar , 2023

Jumla ya Tani 1000 za unga wa mahindi zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni miongoni mwa misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa nchi ya Malawi iliyoathiriwa na kimbunga Freddy ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana janga hilo

Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Ilonda

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, amesema serikali imetoa misaada ya vitu mbalimbali ikiwemo chakula, mahema, na misaada mingine ya kibinadamu na Jeshi hilo ndilo litakalohusika kusafirisha misaada hiyo.

 

"Misaada iliyotolewa ni pamoja na Tani 1000 za unga wa mahindi (Tani 90 kutokea Dodoma na Tani 60 Iringa kuingia Malawi kila siku), Mablanket 6000, na mahema yasiyopungua 50".

Ilonda amesema magari ya JWTZ zaidi ya 37, yataondoka Dodoma muda wowote kuanzia hivi Sasa kupeleka misaada hiyo nchini Malawi.

"Baadhi ya magari hayo yanayopelekwa Malawi ni pamoja na Gari la wagonjwa(Ambulance), Karakana ya magari inayotembea(mobile workshop) na Malori makubwa ishirini yenye uzito wa Tani 30, na malori 10 yenye uzito wa Tani zaidi ya kumi na nane(18), pamoja na Helikopta mbili.

Mnamo Machi 13, mwaka huu kimbunga kiitwacho 'Tropic Freddy' kikiambatana na mvua kubwa na upepo mkali kiliikumba nchi ya Malawi kikisababisha vifo vya mamia ya watu na uharibu wa miundombinu.

Serikali imewatoa hofu wananchi, waonapo shehena ya magari yanayovuka mipaka pamoja na Helikopta kuelekea Malawi zisilete taharuki.