Alhamisi , 17th Sep , 2020

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Profesa Mabula Mchembe, ameitaka mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), kushirikiana na jeshi  la polisi kufuatilia vitambulisho vya wakaguzi  wa mamlaka hiyo ili kubaini wanaoghushi kwa nia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Profesa Mabula Mchembe

Profesa Mabula, ameyasema hayo hii leo Septemba 17,2020, wakati akifanya uzinduzi wa vitambulisho 524 vya wakaguzi vilivyoboreshwa, uliofanyika katika Ofisi za TMDA  Jijini Mwanza, ambapo amesema mamlaka hiyo inajukumu la kufuatilia wakaguzi ili kumlinda mwananchi  na kuhakikisha bidhaa zinakuwa bora kwa matumizi ya binadamu.

"Sera yetu ya wizara kama mnavyoifahamu ni kuhakikisha bidhaa aina ya dawa pamoja na vifaa tiba vinatumika hapa nchini kwa ubora na vikiwa vimethibitishwa usalama wake ili kuwalinda watumiaji", amesema Profesa Mabula.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Adam Fimbo amesema, uwepo wa vitambulisho vilivyoboreshwa utatatua changamoto ya watu wanaojitokeza ambao wamekuwa wakitengeneza vitambulisho bandia  kwa nia ya kuwalaghai wananchi.