Ijumaa , 21st Jul , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini zitatekelezwa, hivyo amewaomba waendelee kuiamini na kushirikiana na Serikali yao.
 

Kauli hiyo imetolewa jana jioni  Julai 20, 2017 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Songwe kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mkuwajuni alipokuwa kwenye ziara ya kikazi, ambapo mbunge wa jimbo la Songwe, Mheshimiwa Philipo Mulugo alimuomba awasaidie kumkumbusha Rais Dkt. Magufuli kuhusu ahadi yake ya ujenzi wa barabara ya lami wilayani humo.
 
Hata hivyo Mhe. Majaliwa amesema kwamba Serikali ya awamu ya Tano ipo makini na imejipanga vizuri katika kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli kama ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 inavyoelekeza.

“Ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli tutazitekeleza, ikiwemo na hii aliyoikumbusha Mheshimiwa Mulugo ya ujenzi wa kilomita nne za barabara ya lami. Tunawaomba wananchi muendelee kuwa na imani na serikali yenu.” Majaliwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bi. Chiku Gallawa akizungumzia hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo alisema watu wanaopata huduma za maji safi na salama katika maeneo ya mijini ni asilimia 42 na vijijini ni asilimia 41.6 na kuongeza kwamba bajeti ya 2017/2018 halmashauri za mkoa huo zimetengewa jumla ya sh bilioni 7.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matanki ya kuvunia maji ya mvua katika majengo yaTaasisi za Umma.

Pia mkoa huo unatekeleza mpango kazi wa usambazaji maji katika maeneo ya mijini na vijijini kwa kupanua mifumo ya usambazaji na kuzijengea uwezo mamlaka za maji na ifikapo Desemba mwaka huu wataongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma hiyo kutoka asilimia 45.04 hadi asilimia 55.63.