Jumatano , 18th Oct , 2017

Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU, Prof. Eleuther Mwageni amesema ufaulu wa wanafunzi wanaoomba kujiunga na vyuo ndio imekuwa changamoto kwenye kuchagua vyuo na kozi za kwenda kusomea.

Prof. Mwageni amesema hayo leo baada ya kufunguliwa kwa awamu ya tatu ya udahili ambayo itawahusu wanafunzi ambao tayari wameshaomba na sio waombaji wapya. Awamu ya tatu imeanza leo Oktoba 18 hadi 22.

Katika kueleza changamoto ambazo tume inakutana nazo kwa waombaji ni namna ya kuzingatia ufaulu wao pamoja na kozi husika sambamba na chuo anachoomba.

“Kwa awamu mbili za awali tatizo kubwa limekuwa ni ufaulu, unakuta mtu ana daraja la kwanza lakini ana ‘C’ tatu mwingine ana daraja hilohilo lakini ana ‘A’ tatu, sasa mkiomba kozi moja na inahitaji watu kumi unafikiri mwenye ‘C’ atachaguliwa halafu mwenye ‘A’ tatu aachwe?, sio rahisi sasa waombaji wanashindwa kuzingatia ufaulu wao na idadi ya watu wanaohitajika kwenye kozi hiyo ndani ya chuo anachoomba”, amesema Mwageni.

Aidha Kaimu Katibu huyo amesisitiza waombaji kutembelea vyuo walivyoomba ili kujua kama wamechaguliwa au la, kisha kuomba tena na kama wamechaguliwa zaidi ya chuo kimoja basi wachague chuo kimoja ili kuirahisishia Tume.