Jumapili , 23rd Apr , 2017

Shule ya Msingi Kitumbi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma inakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na wakufunzi wanne kwa ajili ya wanafunzi zaidi ya 300 hali inayosababisha wanafunzi kukosa masomo stahiki.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitumbi, Igno Ndunguru ameyasema hayo hivi karibuni kuwa shule yake ina wanafunzi 335 lakini ina walimu wanne tu huku mmoja akiwa ni mgonjwa wa muda mrefu.

Nduguru amefafanua tatizo hilo la upungufu wa walimu lipo kwa muda mrefu, hali ambayo inapelekea kushindwa kufundisha wanafunzi hao masomo yote na kwa vipindi  husika kwa madarasa yote kama ilivyopangwa na wizara ya elimu.

Aidha amefafanua kuwa tayari uongozi wa wilaya ulipewa taarifa ya tatizo hilo na kwamba Serikali imesema italitatua itakapoanza kutoa ajira kwa walimu wapya.

 Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Kipapa, Essau Ndunguru naye amekiri  na kudai kuwa ni kero yake ya muda mrefu ambayo kila mara kwenye baraza la madiwani huiwasilisha na kudai kuwa mbali na Kitumbi, tatizo kama hilo lipo pia katika Shule ya Msingi Kihongo.

“Naiomba sana Serikali ione umuhimu wa kuwaleta walimu ili waweze kukabiliana na uhaba katika shule za msingi za kata ya Kipapa kwani mazingira ya utolewaji wa elimu bora kwa wanafunzi ni mbovu sana," alisema Diwani  Ndunguru.

Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Samwel Komba alisema kuwa kwa ujumla halmashauri hiyo ina kabiliwa na tatizo kubwa la walimu kwani idadi ya walimu waliopo ni ndogo sana na kwamba mahitaji ya walimu ni makubwa ambapo kwa mfano shule ya Msingi Kihongo ina wanafunzi zaidi ya 600 lakini ina walimu watano.