Jumatano , 29th Jun , 2016

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha yamvua ubunge wa Longido Onesmo Ole Nangole (CHADEMA) baada ya kubainika dosari wakati wa kuhesabu kura.

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, leo imetengua matokeo ya Ubunge Jimbo la Longido kwa madai kulikuwa na matumizi yasiostahili kutumika kujazwa matokeo ya Ubunge, kwa kutumia fomu namba 21c za kujaza matokeo ya Udiwani na kujaza matokeo ya Ubunge, badala ya kutumia fomu namba 21b.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Silvangilwa Mwangesi aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo amesema hukumu hiyo, iliyosomwa kwa masaa zaidi ya matatu, ambapo Jaji huyo amesema katika uchaguzi huo kulikuwa na dosari nyingi ila dosari kubwa mbili za kujazwa matokeo hayo fomu za udiwani na huku baadhi zikiwa zimefutwa futwa ni tatizo, hivyo anatengua matokeo ya ubunge wa jimbo hilo na kuamuru urudiwe tena.

Alisema kuwa baada ya kutokea dosari hizo, ilitakiwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Longido Felic Kimario aje mahakamani atoe maelezo juu ya uamuzi wa kutumia fomu hizo, lakini alipofika hakuweza kutolea maamuzi, hivyo mahakama imeona ilifanywa kwa makusudi.

Pia mahakama hiyo imethibitisha kuwa kulikuwa na fujo katika uchaguzi huo ambazo zilianzishwa na Onesmo Ole Nangole ambaye ni Mbunge wa sasa katika chumba cha majumuisho, hivyo inatengua ubunge wake.

Jaji Mwangesi aliamuru taarifa za kutenguliwa ubunge huo zipelekwe Tume ya Uchaguzi haraka na kwa msimamizi wa Uchaguzi Longido, ili aweze kuandaa uchaguzi mwingine, ikiwa na kuutaka upande wa Chadema kulipa gharama za kesi hizo.

Mahakama ilitupilia mbali madai ya kuwepo lugha za kashfa kwa Dk. Steven Kiruswa, suala la wakenya na kutumika kwa magari ya CHADEMA kubeba masanduku ya kura.

Katika kesi hiyo upande wa mdai Dk. Steven Kiruswa, alitetewa na Dk. Masumbuko Lamwai akisaidiana na Edmund Ngemela na Daud Haraka, huku upande wa Mdaiwa wa kwanza Onesmo Ole Nangole wa Chadema, akitetewa na wakili Method Kimomong'olo akisaidiana na John Materu.

Upande wa mdaiwa wa pili ambao ni Mwanasheria Mkuu wa serikali ukiwakilishwa na Daud Akway akisaidiana na Neema Nyanda.

Miongoni mwa madai yaliyopo katika kesi hiyo ni magari ya Chadema kudaiwa kutumika kubeba masanduku ya kura, Mgombea wa CCM Dk. Steven Kiruswa kutolewa lugha ya matusi wakati wa kampeni, kuwa yeye sio mmasai ni Mmarekani na anafanya kazi Marekani, pamoja na baadhi ya wapiga kura wakenya kupigia kura Chadema.

Kwa upande wa Mbunge aliyetenguliwa Onesmo Ole Nangole, amesema hakubaliani na hukumu hiyo na atakata rufaa.