Jumanne , 9th Aug , 2022

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amemuhakikishia Rais wa wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza maagizo aliyoyatoa ya kuhakikisha migogoro ya mipaka baina ya wananchi na Hifadhi za Taifa inatatuliwa haraka

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo, Wilayani Makete mara baada ya . Rais Samia kutaka kujua hali ya mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Kitulo na wananchi wanaopakana na hifadhi hiyo.

Aidha, ameeleza kuwa licha ya kazi kubwa inayoendelea kufanywa na kamati  inayojumuisha Mawaziri 8 ya kutatua  migogoro, Wizara anayoiongoza ipo katika hatua nzuri ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu ikiwashirikisha Wananchi na Serikali ya Wilaya.


Waziri Balozi Dkt. Chana ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanazingatia na kuheshimu makubaliano na mipaka  iliyowekwa ili kuepuka kuibua migogoro mipya inayodhoofisha shughuli za uhifadhi wa Rasilimali adhimu za Urithi wa Utalii.
Rais Samia Suluhu Hassan yupo mkoani Njombe kwa ziara ya kikazi ya Siku mbili ambapo moja ya mambo aliyoyafanya ni pamoja na kufungua Barabara ya Makete Njombe.