Jumanne , 22nd Jul , 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi katika Mkoa wa Ruvuma kushindwa kumaliza shule kwa hatua mbali mbali kwa sababu mbali mbali ukiwemo utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.

Rais Kikwete katika moja ya shule mkoani Ruvuma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi katika Mkoa wa Ruvuma kushindwa kumaliza shule kwa hatua mbali mbali kwa sababu mbali mbali ukiwemo utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.

Utoro na mimba za wanafunzi ni mambo ambayo yamezunguzwa kama changamoto za Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, na Mbunge wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, wakati alipozungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Rais Kikwete kwenye Uwanja wa Michezo wa Namtumbo jioni ya leo, Jumatatu, Julai 2014.

Kwa mujibu wa takwimu za tatizo la mimba katika Mkoa wa Ruvuma, kiasi cha watoto wa kike 155 wameshindwa kumaliza masomo yao ya shule za msingi na sekondari katika miezi 18 iliyopita kwa sababu ya kupata mimba.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Mwaka 2013, watoto 16 za shule za msingi na wanafunzi 78 wa shule za sekondari walikatisha masomo kwa mimba wakati mpaka mwezi uliopita kwa mwaka huu, wasichana watano wa shule za msingi na 56 wa shule za sekondari waliacha shule kwa sababu ya kupewa mimba.

Changamoto ya utoro nayo ni kubwa katika Mkoa wa Ruvuma. Takwimu za utoro zinaonyesha kuwa kati ya watoto 41,801 walioanza shule ya msingi Mwaka 2007 ni watoto 30,698 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi Mwaka 2013. Hii ina maana kuwa asilimia 26.56, sawa na watoto 11,103 hawakumaliza shule ya msingi kwa sababu ya utoro.

Kwa upande wa sekondari, kati ya wanafunzi 18,892 walioingia sekondari Mwaka 2010 ni wanafunzi 9,968 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana. Kiasi cha wanafunzi 8,924, sawa na asilimia 47.23, hawakumaliza masomo ya sekondari kwa sababu ya utoro.
Kwa Wilaya ya Namtumbo pekee, kati ya wanafunzi 2,739 walioingia kidato cha kwanza Mwaka 2010, ni wanafunzi 997 tu waliomaliza kidato cha nne mwaka jana. Wanafunzi 1,742, sawa na asilimia 63.59, hawakufanya hata mtihani wa kumaliza kidato cha nne.
Takwimu hizo zimemsitikisha Rais Kikwete ambaye ameeleza waziwazi masikitiko yake akisisitiza: “Hali ya shule za msingi ni mbaya, hali ya sekondari mbaya. Wako wapi watoto hawa wanaostahili kuwa shule? Kwa nini hawako shule? Na wanafanya nini badala ya kuwa shule? Hali hii ni mbaya, mbaya, mbaya, ni aibu kubwa sana hii.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Suala hilo nalirudisha kwenu nyie Madiwani. Kuweni makini hawa ni watoto wenu. Nataka kila miezi sita mpatiwe ripoti ya mahudhurio ya wanafunzi katika shule zote za mkoa huu. Na kila mwezi, wakuu wa shule zote nchini watoe taarifa za mahudhurio ya wanafunzi kwa maofisa elimu. Pia Kamati za Maendeleo ya Jamii za Halmashauri nazo lazima zidai ripoti za mahudhurio kutoka kwa wakuu wa shule.”

Rais Kikwete pia amewaagiza viongozi kushirikiana na vyombo vya sheria mkoani na wilayani kukabiliana na tatizo hilo kubwa.
Kuhusu malalamiko ya wananchi wa Wilaya ya Namtumbo ya kuibiwa fedha zao za zao la tumbaku na kushindwa kulipwa kwa miaka miwili sasa, Rais

Kikwete ameagiza viongozi wote ambao ripoti ya Mkuu wa Mkoa inaonyesha kuwa walishiriki katika wizi huo, wakamatwe na kufikisha mbele ya sheria.

“Hawa watu wanawadhulumu watu. Wanawafanya kama watoto wadogo. Hili jambo lisipelekwe kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Maendeleo ya Ushirika ama kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushiriki – ripoti ya Mkuu wa Mkoa ipelekwe polisi kwa hatua za kisheria. Siyo kazi ya Wizara ama Mrajisi kuamua nani ashitakiwe kwa wizi. Wezi wanashtakiwa na Jamhuri,” ameagiza Rais Kikwete na kuongeza:
“Na nyie wananchi acheni kuchagua wezi kuongoza ushirika. Mnachagua wezi na wakishawaibieni mnaanza kulaumu Serikali na CCM – badala ya kukabiliana na kukamata wezi, mnalifanya jambo hili suala la kisiasa.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Chama cha Ushirika ni chenu, pesa iliyoibiwa yenu, viongozi wa ushirika mmewachagua wenyewe, sasa kwa nini mnalaumu watu wengine. Mnaruhusu watu watakate kwa jasho lenu. Kataeni wizi huu na wafikisheni wezi polisi…habari ndiyo hiyo.”