Jumanne , 21st Mar , 2017

Serikali imefuta usajili wa vibali vya uzalishaji na Uingizaji wa aina 20 ya pombe kali za viroba zilizokuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Maboksi ya pombe za viroba

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam kuhusu usitishaji wa uzalishaji na uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe zilizofungwa katika mifuko ya plastiki (Viroba).

Waziri Ummy amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa Februari 02, 2017 la kusitisha uzalishaji, uingizaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hiyo kali kuanzia Machi 01, 2017 na zitahusu matumizi ya pombe kali zilizofungashwa katika mifuko ya plastiki (viroba) chini ya ujazo wa milimita 200.

Aidha amesema kuwa uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya pombe za aina hiyo unatokana na athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya na kijamii ambapo matumizi mabaya ya pombe hizo yamesababisha  ajali nyingi, vifo, ulemavu na mzigo mkubwa kwa Serikali wa kutoa huduma kwa wahanga wa pombe hizo na ongezeko la makosa ya jinai.