Jumapili , 29th Nov , 2020

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewataka wamiliki wote wa ardhi walio na viwanja visivyoendelezwa na kulipiwa kodi ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipia viwanja vyao ndani ya siku kumi na nne, baada ya kupokea ankara ya madai na wasipotekeleza watanyanganywa viwanja vyao.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami (kulia) na wataalamu wengine wakichukua mawasiliano kutoka kwa kijana aliyemkuta katika nyumba iliyopo eneo la Chidachi jijini Dodoma wakati wa zoezi la kupita nyumba kwa nyumba kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa wiki.

Aguizo hilo limetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Denis Masami wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika Mtaa wa Chidachi Jijini Dodoma ikiwa ni Mkakati wa Wizara kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati.

‘’Maeneo mengi nchini yana viwanja visivyoendelezwa na wakati huo wamiliki wake hawavilipii kodi ya pango la ardhi jambo linaloikosesha mapato serikali, baada ya siku kumi na nne tutaanza utaratibu wa kuvitwaa, kuvinadi ili kufidia deni na kumilikishwa kwa watu wengine,’’ amesema Masami.

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi, ameongeza kwa kusema kuwa, wizara inatekeleza mkakati wake wa kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kushirikisha wataalamu wa sekta ya ardhi na Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika mikoa kwa kupita nyumba kwa nyumba na kuwapelekea wadaiwa ankara za madai ya ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine yatokanayo na sekta ya ardhi ili waweze kulipa.