Alhamisi , 19th Jan , 2017

Wahamiaji haramu 11 kutoka nchini Somalia leo wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha Sheria.

 

Waendesha Mashitaka wa Serikali kutoka idara ya uhamiaji,Jamila Ilomo na Aranyakira Kitosio, wamedai mahakamani hapo jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Januari 11 mwaka huu, katika nyumba ya kulala wageni ya Olasiti, iliyopo eneo la Olasiti jijini Arusha.

Katika kesi hiyo namba 22 ya mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nestory Barro, Jamila amedai kuwa watuhumiwa hao waliingia nchini kinyume na Sheria ya uhamiaji.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohamed Hassan (33), Said Omarisobla(22), Ally Abubakar(20), Mahad Ali Haashi(19), Sharif Khalif(18), Abdinasir Hassan Nur(22), Naima Abdala(23), Hudhan Abdi(18), Maimuna Ahmed (19), Mruaya Ahmed(28) na Irene Athuman(19).

Watuhumiwa hao walikiri kufanya kosa hilo na kesi hiyo kuahirishwa hadi Februari Mosi mwaka huu.