Ijumaa , 21st Jul , 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia biashara ya mazao mbalimbali katika maeneo yao ili wakulima waweze kupata tija.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Majaliwa ametoa agizo  hilo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ilasilo kilichoko katika mpaka wa mkoa wa Mbeya na Songwe alipokuwa njiani kuelekea wilayani Songwe kwa ajili ya ziara ya kikazi.

"Wakulima msikubali kuuza mazao ovyo, wekeni na akiba ya chakula, pia  Bodi ya mazao mchanganyiko itakuja hapa kwa kuwa sasa inapita sehemu mbalimbali kupata taarifa za bei za mazao pamoja na kuwatafutia masoko yenye tija", amesema Majaliwa.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu amewaagiza watu wote wanaohusika na suala la usambazaji wa pembejeo kuhakikisha wanazifikisha kwa wakulima katika kipindi kisichopungua muda wa miezi miwili kabla ya kuanza kwa msimu ili kuwaondolea changamoto ya uchelewashwaji wa huduma hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bi. Chiku Gallawa ametaja changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo ni pamoja na kutokuwepo kwa soko la uhakika la mazao  na uingizwaji wa pembejeo zisizofaa katika mkoa.