Jumapili , 29th Jan , 2023

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, Mary Masanja amewahimiza wananchi kuwa wahifadhi wa mazingira kwa kupanda miti ili kuepukana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoikumba dunia kama ukame na mafuriko

Ameyasema hayo leo katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama cha Mapinduzi yanayotarajia kufikia kilele chake Februari 5, 2023

“Nataka niwakumbushe kwamba uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo tuyatunze mazingira ili yaweze kututunza” amesisitiza Mhe. Masanja

Ameongeza kuwa Ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kila mwananchi ahakikishe anapanda mti na kuutunza ili uweze kukua.

Amesema kufuatia  maelekezo hayo  ya Mheshimiwa Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii imehakikisha inatumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kupanda miti hususan katika kipindi hiki cha mvua kwenye maeneo mbalimbali ya nchi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa ya kijani.

Amefafanua kuwa Mheshimiwa  Rais Samia amekuwa kinara wa kuhifadhi mazingira na mwongoza njia katika uhifadhi na pia yeyendiye muasisi wa  filamu ya The  Royal tour iliyopelekea kila mtu sasa anajua masuala ya utalii na uhifadhi.

Mhe. Masanja amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo katika jiji la Mwanza mathalani fedha za ujenzi wa barabara, meli, daraja la kigogo Busisi na miradi mingine ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja ametembelea Shule ya Sekondari Muhandu iliyopo katika Halmashauri ya jiji la Mwanza kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi na wananchi wa eneo hilo kuwa na utamaduni wa kupanda miti.
Akiwa katika shule hiyo, Mhe. Masanja amewahimiza wananchi kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na   Chama cha Mapinduzi ( CCM).

“CCM  ndicho chama  kinachoongoza nchi hivyo tukiunge mkono ili kuwaletea wananchi maendeleo  kwa hiyo pia tumuunge mkono Mheshimiwa Rais ili tuweze kufikisha maendeleo ya wananchi pale mlipo” amesema Mhe. Masanja.

Maadhimisho ya Miaka 46 ya Chama cha Mapinduzi yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda ambaye alikuwa mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti UWT Taifa, Zainab Shomari pamoja na viongozi wengine wa UWT Taifa na wanachama wa jumuiya hiyo kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania.