Alhamisi , 25th Feb , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amesema kuwa serikali haichukii watu wanaoipa changamoto na wanaokosoa kwa staha na kuwataka Watanzania watangulize uzalendo kwani si kila kitu cha kuweka mitandaoni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli

Rais Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo leo Februari 25, 2021, wakati akizungumza katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika soko la kisasa la Kisutu pamoja na kuzindua jengo la Jitegemee na studio za Africa Magic Group Limited.

"Serikali haichukii wanaotupa changamoto na kukosoa kwa staha, kitakwimu tumeruhusu vyombo vingi sana vya habari katika kipindi hiki kuliko wakati wowote tangu tupate uhuru, sasa tuna vituo vya Radio 193 na vya TV vipo 46," amesema Rais Dk. Magufuli.

"Nitoe wito kwa wanahabari na Watanzania, vyombo tunavihitaji na habari tunazihitaji lakini tutangulize uzalendo na haki ya yule anayeandikiwa habari, pamekuwa na habari nyingi za uzushi mara fulani kafa mara vigogo wapukutika ni mambo ya ajabu," ameongeza kusema Rais Dk. Magufuli.