Alhamisi , 17th Sep , 2020

Watu watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano ikiwemo kosa la uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha Dola za Marekani zaidi ya laki tatu zaidi ya milioni 70 za kitanzania, mali ya kampuni ya SMCI ya Marekani.

Washtakiwa hao Deogratius Masika, William Kimonge wakazi wa Dar es salaam na Youssoufa Sabo raia wa Cameroon wamesomewa shitaka lao  mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi Cassian Matembele.

Inadaiwa kati ya Desemba 2016 na Januari 2017 jijini Dar es salaam, waliilaghai kampuni ya SMCI ya Marekani na kujipatia dola za Marekani  laki tatu na ishirini wakidanganya kuwa wataisambazia kampuni hiyo tani elfu tano za korosho kutoka Mtwara wakati sio kweli.

Katika shtaka la tatu na la nne ambalo ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,  washtakiwa hao wanadaiwa kuilaghai Kampuni ya SMCI ya nchini Marekani na kujipatia Dola elfu kumi na tano za Marekani wakidanganya kuwa wataisambazia kampuni hiyo tani elfu kumi za korosho kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, wakati sio kweli.

Aidha washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la kuilaghai Kampuni hiyo na kujipatia Dola za Marekani zaidi ya  laki tatu na kuziingiza kwenye Account ya CRDB yenye jina la JAW distributors limited, kwa lengo la kubadilisha kuwa fedha za Kitanzania.

Hata hivyo washtakiwa hao wamekana shtaka linalowakabili huku Hakimu anayeendesha shauri hilo kudai dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa namba mbili ambaye ametakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya milioni sitini na tisa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septamba 29 mwaka huu na washitakiwa wote wamerudishwa rumande