Jumatatu , 21st Aug , 2017

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu amekiri kuwa nchi ya Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mahabusu za watoto ambapo kwa sasa kuna vituo vitano tu.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo wakati akikabidhiwa kisima cha maji safi kilichojengwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam kwa ajili ya kuwasaidia watoto na wafanyakazi wa mahabusu ya watoto Upanga.

Waziri Ummy amesema changamoto hizo serikali imeziona na tayari mipango madhubuti imekwisha andaliwa ili kumaliza hali  ya kuwachanganya watoto na watu wazima ambayo siyo sahihi.

Katika hatua nyingine Mhe. Ummy amesema kisima hicho alichokabidhiwa leo kitazalisha lita 5,000 kwa siku na kuokoa gharama za kila mwezi kwa serikali ambazo zilikua zinatumika kulipia huduma hiyo ambapo fedha hizo zitabadilishwa matumizi kwa kuwafungulia bima za afya.

Kwa upande wa Kadinali Pengo kwa upande wake amesema katika misaada yao ambayo wamekuwa wakiitoa kwa jamii wanaepuka kuitoa kwa ubaguzi wa aina yoyote.

"Tunaweza kufanya hayo japo yanaweza kuonekana ni madogo lakini sisi tunasukumwa na upendo, hivyo tukifika mahali hatuulizi wewe ni dini gani au dhehebu gani tunapenda amani na upendo udumu kwenye jamii,"alisema

Chanzo cha kuchimbwa kisima hicho ni kutokana na ziara waliyoifanya watoto wa Shirika la Utoto Kurasini kituoni hapo na kubaini changamoto inayowakabili watoto wenzao, hivyo wakaguswa na kuomba ushirikiano na vikundi vingine vilivyowezesha kujengwa kwa gharama ya Sh 11,780,000.