Alhamisi , 19th Jan , 2017

Serikali imezipa msisitizo wizara mbalimbali kuhakikisha zinahamishia makazi yake Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma kabla ya Februari 28, mwaka huu, kama iliyotangazwa na Rais John Magufuli mwaka jana.

Waziri Jenista Mhagama wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa wanachama wote wa Saccos ya Makamu Savings and Credit iliyopo chini ya ofisi ya Wziri Mkuu, leo Mjini Dodoma

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema agizo la serikali lazima liwe limetekelezwa ifikapo Februari 28, mwaka huu.

“Kama agizo lilivyotolewa na Rais Magufuli kuhusu wizara na watumishi wake kuhamia Makao Makuu Dodoma, ndivyo wanavyotakiwa manaibu makatibu wakuu, makatibu, manaibu mawaziri na mawaziri kutakiwa kuwapo Dodoma mwishoni mwa Februari,” alisema Mhagama.

Waziri Mhagama alisema ofisi yake imeweza kukagua miundombinu na ujenzi wa majengo mbalimbali ya serikali yanayoendelea kujengwa na mengine yakiwa yamekamilika kwa ajili ya matumizi ya wizara hizo.

“Hakuna tatizo la ofisi za watumishi wa wizara zote, kwani majengo yamekamilika na yapo katika hali nzuri tayari kwa ajili ya kuanza kutumiwa, hivyo wakuu husika wakiwamo mawaziri wahakikishe wanatakiwa kuhamia Dodoma,” alisema.