Jumapili , 20th Aug , 2017

Jeshi la Polisi Kauti ya Siaya  nchini Kenya limeutaka umma kuacha polisi kufanya kazi yao juu ya uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa  msimamizi msaidizi katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliofanyika Agosti 8 baada ya mwili wake kukutwa akiwa ameshafariki. 

Mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Siaya, Sarah Duncan alisema uchunguzi unaendelea na upelelezi wa awali unaonesha kuwa marehemu aliyejulikana kwa majina Caroline Odinga alibakwa na watu wengi na sehemu zake za siri pamoja na sikio moja kukatwa vibaya.

Mkuu huyo wa polisi alisema pia Mwili huo ulikutwa katika soko la Sega Jumamosi asubuhi na watu waliokuwa wakielekea katik amazishi ya Mkurugenzi wa TEHAMA wa IEBC, Chris Msando katika kijiji cha Lifunga.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo taarifa zinasema kwamba Familia ya Bi. Odinga inadai kuwa mara ya mwisho marehemu alitoka nyumbani akielekea kudai malipo yake kwa kazi aliyofanya ya usimamizi katika uchaguzi mkuu ulioisha.

Bi Odinga ambaye pia ni Mwalimu wa Ugenya High School alikuwa msimamizi msaidizi akifanya kazi na IEBC katika uchaguzi Mkuu wa Kenya mnamo Agosti 8 mwaka huu.