Alhamisi , 30th Mar , 2017

Meneja wa Msanii Snura, HK amesema yeye pamoja na msanii wake hawana 'bifu' na Shilole huku akidai wapo tayari hata kufanya naye kazi ya pamoja endapo atakuwa anahitaji katika hilo.

Hayo yamekuja baada ya tetesi za muda mrefu zikiwahusisha wadada hao wawili kwa kile kilichowaaminisha mashabiki katika nyimbo zao kujawa mafumbo huku wengine wakiyatafsiri ndivyo sivyo.

"Mimi nafikiri bifu ya Shilole na Snura zinatengenezwa na mashabiki wenyewe kutokana hawa wote walitoka kwenye bongo muvi wakaja kwenye bongo fleva, alianza Shilole akaja Snura. Wote wakatusua katika kipindi kimoja, yule ametoa 'Paka wa Baa' ina-hit kule Snura anatoa 'Majanga' nayo ina-hit kwa hiyo wakakutana katika 'game' watu wakawa wanafananisha kulingana na walipotoka lakini siyo wana bifu mpaka inafikia hatua hawaongei siyo kweli". Alisema HK katika kipindi cha eNewz kinachorushwa na EATV.

HK

Aidha meneja huyo amesema ameshawahi kuwaona mara nyingi wanadada hao wakiwa pamoja wanasalimiana na kuongea.

Kwa upande mwingine HK amesema yupo tayari yeye na msanii wake kufanya kazi pamoja na Shilole endapo atakubali muda wowote milango ipo wazi katika suala hilo.