Jumamosi , 22nd Oct , 2016

Mkali wa muziki wa uswazi, anayejiita 'Mfalme wa Uswahili' Msaga Sumu amesema ngoma yake mpya aliyoipa jina la 'Iga Tena' siyo dongo kwa mtu yeyote, bali ni ujumbe wa kawaida unaotokana na maisha kila siku ya watanzania.

Msaga Sumu, akiwa ndani ya FNL

Msaga Sumu ambaye amejitambulisha katika game kupitia muziki wa singeli ametoa ufafanuzi huo wakati akiitambulisha rasmi video ya wimbo huo, kupitia kipindi cha FNL, cha EATV, na kuongeza kuwa huo ni ujumbe kwa watu wote ambao wamekuwa na kawaida ya "kukopi" vitu vya watu bila kuumiza vichwa wala kutambua kazi ya muanzilishi.

Akizungumzia video hiyo, Msaga Sumu amesema ameamua kuwa serious katika muziki na ndiyo maana amefanya kitu kikubwa zaidi katika video hiyo ambayo ameonesha mazingira halisi ya uswahilini.

Kuhusu yeye kufunikwa na baadhi ya wasanii wa singeli walioshika chati hivi sasa, Msaga Sumu ameendelea kusisitiza kuwa yeye ndiye baba wa muziki wa singeli na hakuna mtu atakayeweza kumfunika.

Amesema ameitoa mbali singeli tangu enzi za vigodoro kiasi cha kutishiwa kupelekwa mahakamani na baadhi ya wasanii wa taarab, kwa madai kuwa alikuwa akitumia muziki wao, na kuingiza sauti yake.

"Mimi ndiye mwanzilishi wa singeli, nimeipigania sana toka enzi za vigodoro kabla havijapigwa marufuku, nilikuwa na loop beat za taarabu hadi akina Mzee Yusuph wanataka kunishtaki, nimepigana hadi leo hii imefikia hapa" Amesema Msaga Sumu.

Katika hatua nyingine amedai kuwa yeye ndiye aliyekiibua kipaji cha Shlo Mwamba kwa kumpa nafasi katika kazi zake

"Nilikuwa nikipata kazi nashirikisha wanagu kibao ili nao waonekane, nakumbuka kwa mara ya kwanza mimi ndiye nimemtambulisha Sholo mwamba, nilikuwa na kazi fulani, nikampigia simu, akaja, nikampa nafasi akashika kipaza akafanya mambo, na watu wakaanza kumjua"

Sholo Mwamba (Kushoto) akiwa na Prof Jay katika video ya Kazi