Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva ambaye msimu huu ameifungia klabu yake jumla ya mabao 14 amefunguka kwamba, msanii Alikiba anaitendea haki nchi yake ya Tanzania kwa kazi ya muziki ambapo amekuwa akifanya kazi bora zinazoleta sifa kwa nchi.

Msuva amesema hayo leo kupitia kwenye kipindi cha Planet bongo ya East Africa Radio na kusema yeye anamkubali sana msanii huyo kutokana na uwezo wake kimuziki na namna anavyoweza kuimba vizuri kila apatapo nafasi. 

"Kwanza naupenda sana ule wimbo wa wale jamaa wa Kenya wameshirikisha Alikiba 'Unconditionally Bae', naukubali ule wimbo sababu watu wamepangilia sana kazi yao mle ndani na unayasikia kabisa, nimependa mavazi ya mule jinsi walivyovaa ni mavazi fulani ambayo yanawakilisha Afrika japo hata watu wa Ulaya wanavaa lakini naona Afrika watu wanapenda sana kuvaa vile" alisema Msuva 

Msuva aliendelea kutoa ufafanuzi juu ya wimbo huo na uwezo wa Alikiba 

"Ukisikiliza ule wimbo unaona jinsi ambavyo Alikiba amefanya vizuri yaani ameitendea haki Tanzania maana ametuwakilisha vizuri Tanzania yetu, kuwa tunaweza kuimba pia tunaweza hata kuwashirikisha nyinyi wenyewe mkaja kucheza nyimbo zetu huku Tanzania"- alisema Simon Msuva.