Jumatatu , 1st Sep , 2014

Tamasha la Kili Music Tour linalodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager limeacha gumzo kub

Tamasha la Kili Music Tour linalodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro Premium Lager limeacha gumzo kubwa Tanga huku wasanii walioshiriki ziara ya muziki ya Kilimanjaro, inayotia nanga wiki hii katika viwanja vya Leaders kwa nyakati tofauti wamekiri kwamba kila mmoja kwa njia yake amejifunza makubwa katika ziara hiyo ambayo wengi wameitaja kuwa ni ziara namba moja kwa ubora.

Wakiongea na waandishi wa habari kwa nyakati tifauti mara baada ya kushuka jukwaani wasanii hao wameisifu ziara hiyo kwanza kwa kuwa ni ziara inayowaweka wasanii kwenye hadhi lakini pia ni ziara ambayo ina mpangilio wa kueleweka.

Waliongea katika tamasha kubwa lililofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani ambapo maelfu ya mashabiki waliitokeza na kupata burudani ya aina yake iliyodumu zaidi ya saa saba huku ikiwa na msisimko kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Kwa upande wake Omary Nyembo, au Ommy Dimpoz kama alivyozoeleka kuitwa na mashabiki wake, amesema Kili ni ziara iliyomuweka karibu na mashabiki wake wa kipato cha chini baada ya kuwa na ziara yenye viingilio vya chini iliyohusisha wasanii wakuwa nchini.

Rich Mavoko, nyota wa wimbo unaotamba sasa hivi wa Roho yangu amewaambia waandishi kwamba mwisho wa ziara hii ndio mwanzo wa kujipanga kwake kwa ajili ya ziara ya mwakani ambapo ameahidi kurudi vingine huku akiwa ameongeza nguvu katika utendaji wake jukwaani.

Joseph Haule au Profesa Jay aliisifia ziara hiyo na wadhamini wake, Kilimanjaro Premium Lager kwa kuandaa ziara ya kizalendo ambayo imekuwa ikizunguka nchi nzima kuwanadi wasanii wa nyumbani na kuwakutanisha na mashabiki wao bila kuangalia faida, bali kuhakikisha muziki nwa kitanzania unafika katika kilele cha mafanikio.

Kundi la muziki la weusi lililo na wanamuziki watatu ambao ni Joh Makini, Nikki wa Pili na G Nako, wakiwakilishwa na msemaji wao Nikki wa Pili kwa upande wao wameishukuru kampuni ya Bia Tanzania kwa kuwapa nafasi ya kupanda katika majukwaa ya mikoa yote Tanzania ambapo wamefanikiwa kuwaonesha mashabiki wao uwezo wao kikazi lakini pia wameweza kujenga mahusiano na wadau.

Wasanii walioshiriki tamasha hilo ni pamoja na Ommy Dimpoz, Rich Mavoko, ben Paul, Khadija Kopa, Mzee Yusuph, Profesa Jay na Weusi.

Kili Music Tour inaratibiwa na East Africa Radio na Tv, Executive Solutions, Integrated Communications, Aggrey & Clifford na Aim Group.

Baada ya kuzunguka mikoa tisa, Jumamosi ijayo ni zamu ya Dar es Salaam ambapo ziara hii itahitimishwa kwa kishindo.