Alhamisi , 19th Jan , 2017

Msanii wa nyimbo za Injili Madam Flora (Zamani: Flora Mbasha) amesema mwaka huu utakuwa ni wa mwisho kwake kutoa albam na kwamba atakuwa anaachia single nyingi ili aweze kuwapatia mashabiki zake nyimbo  nyingi mara kwa mara.

Madam Flora

Utaratibu wa albam umepotea kwa muda mrefu katika tasnia ya burudani nchini (Tofauti na muziki wa injili) kwa madai kuwa hazina soko, licha ya baadhi ya wasanii hivi sasa likiwemo kundi la Navy Kenzo na Ditto kutangaza kuanza kuurejesha taratibu kwa kutoa albam zao mwaka huu.

Akiongea kupitia eNewz Flora amesema kuwa  hiyo ndiyo 'plan' yake kwa miaka ijayo huku akitaka mashabiki wanamuona kuwa amekuwa kimya kwa muda mrefu kutambua kuwa muziki wa Injili upo tofauti na muziki wa bongo fleva ndiyo maana inakuwa rahisi kwa wasanii wa bongo fleva kuachia nyimbo mara kwa mara.

Amesema nyimbo za Injili zinahitaji kuwa na muda wakutosha na kumuomba Mungu ili akupatie mashairi mazuri yenye ujumbe ukisema ukurupuke na kuachia nyimbo kila siku utajikuta unatoa albamu nyingi lakini hit song ni moja na nyimbo nyingine zinasindikiza.