Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Mtayarishaji Mkongwe wa muziki bongo P Funky Majani amefunguka na kutetea kauli ya Harmorapa kutomfahamu Master J na kudai yawezekana ikawa kweli hafahamiki kwa kuwa amejikita zaidi kwenye Ku-jaji mashindano ya BSS kuliko muziki.

Akizungumza kwenye heshima ya Bongo Fleva  ndani ya Planet Bongo East Africa radio, Majani amesema kuwa Harmorapa ameibuka kipindi ambacho Master J amepumzika kutengeneza muziki hivyo ni kweli inawezekana asifahamike na kizazi cha kina Harmorapa na wengine wachanga waliopo

Pamoja na hayo Majani ameongeza kuwa wasanii wengi wamekuwa wakimtambua yeye kama 'Prodyuza' mkongwe kwenye muziki wa bongo kwa sababu alipambana kuusimamisha muziki wa bongo fleva na kugeuka kuwa sehemu ya biashara na kazi yenye heshima.

"Inawezekana kweli Harmorapa hamfahamu Master J, siwezi kumlaumu kwa hilo kwa sababu kwa muda mrefu watu wanamuona kama jaji wa mashindano, lakini mimi najulikana zaidi kwa kuwa na hits nyingi sokoni hivyo Harmorapa yupo sahihi. Lakini Master J anamchango wake mkubwa tu kwenye hii tasnia ya ya muziki na ni rafiki yangu mkubwa sana sema hii generation ya kina Harmorapa yaweza kuwa wasimtambue kama prodyuza bali jaji"- Majani aliwaambia watangazaji wa Planet Bongo.

Pamoja na hayo Majani amejinadi hajawahi kupata ushindani wowote wakati anafanya kazi za utatarishaji wa muziki kwani katika chati za redio na televisheni alikuwa anaongoza kwa kuwa na nyimbo kali nyingi zinazofanya vizuri.