Jumatatu , 21st Aug , 2017

Rapa Mwana FA, a.k.a The Choir Master amewataka wasanii wenzake wawe na mapenzi ya dhati katika kile wanachokifanya ili kiweze kuwaletea manufaa zaidi nasiyo kutegemea kiki kuliko muziki wao.

Rapa Mwana FA, a.k.a The Choir Master.

Mwana Fa amebainisha hayo baada ya wasanii wengi kufahamika zaidi kupitia skendo mbalimbali kuliko hata muziki wake ambao anaoufanya kama kazi yake kila siku.

"Kitu cha kwanza ninachokitaka kwa wanamuziki wawe na mapenzi na muziki, maana tunakosea sana tunavyofanya muziki biashara kwa kutegemea muziki utuletee pesa tu na umaarufu bila ya kuwa na mapenzi kwenye muziki wenyewe. Ndiyo maana tunaona makiki yanazidi kuliko muziki tunaofanya, yaani watu wanafanya matukio yanawapa umaarufu lakini ukija kuulizia kazi zake huzijui alizofanya", alisema Mwana FA.

Pamoja na hayo, Mwana FA amesema kwa upande wake aina ya muziki anaoufanya ndiyo unapelekea kutofanya 'collabo' nyingi na wasanii wa kimataifa.

"Naamini kuna soko kubwa sana hapa Tanzania, naona jinsi nguvu nyingi zinazotumika kujaribu labda kuupeleka muziki wetu nje ya mipaka yetu. Siwezi kuzika hili ni soko langu naamini hata bado sijalimaliza, soko letu lipo hapa hapa hizi nyingine zinakuwa mbwembwe tu kufanya kazi na wasanii wa nje ili tutishie wasanii wa ndani kwamba mimi nimeshakuwa mkubwa naweza kukaa katika nyimbo moja na msanii fulani. Kwa hiyo kama naweza kuwafikia watu, naweza kutengeneza namba moja 'hits song' bado sina presha zikitokea sawa sina stress nazo".

Kwa upande mwingine, Mwana FA amewashauri wasanii wenzake watengeneze nyimbo zilizokuwa bora ili ziweze kusikilizwa na kila mtu bila ya kubagua mtu wa kusikiliza.