Jumatano , 26th Jul , 2017

Rapa Chemical baada ya kuonekana kwenye muonekano mpya hivi karibuni, amefunguka mapya na kusema yeye kuonekana amevaa nguo za kuogelea siyo kitu cha ajabu kwake kwani akiachana na muziki uliomtambulisha uigizaji ni kipaji cha pili alichojaaliwa.

Chemical amesema ingawa amewashtua mashabiki zake ambao wengi wao hawakutegemea kumuona akivaa nguo kama alivyoonekana kwenye video aliyoshirikishwa na Msami Baby 'So Fine',  amewatoa hofu mashabiki zake na kwamba anauwezo wa kuvaa uhusika wa aina yoyote haswa ikiwa suala la sanaa.

"Kitu ambacho watu wanapaswa kujua mimi ni muigizaji. Ukiachana na muziki ulionitambulisha kwenye jamii ya Tanzania naweza kufanya kitu kingine chochote kinachohusiana na sanaa. Mavazi niliyovaa hayajanipa tabu kwani niliyakuta location nikaambiwa nivae na kwa sababu Msami aliangalia suala hili haswa kibiashara zaidi sikutaka kumfelisha. Chemical anabadilika kutokana na Mazingira" alisema.

Kwa upande wa Msami ambaye ndiye aliyetoa wazo la kubadilisha muonekano wa Chemical amesema alitaka kuonyesha uwezo wa Chemical katika utofauti uliozoeleka.