Jumatatu , 27th Mar , 2017

Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa msanii Nay wa Mitego unaojulikana kwa jina la 'Wapo' kutumika kwa namna yoyote ile kuanzia leo kutokana na kutokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa na baraza hilo.

Katibu Mkuu wa Baraza hilo Bwana Geofrey Mngereza (kushoto) na Msanii Nay wa Mitego

Katibu Mtendaji wa baraza hilo Bwana Geofrey Mngereza ametoa tamko hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa wananchi na wadau kuacha kutumia kazi zilizopigwa marufuku kwani wakibainika hatua kali dhidi yao itachukuliwa.

“Kwa wale ambao watabainika wanatumia kazi hizi zilizopigwa marufuku ikiwa katika radio stesheni, bodaboda, mtaani hata katika ‘club’ hatua kali zitachukuliwa  dhidi yao kwa sababu wanaendelea kutumia vitu ambavyo vimefungiwa na baraza”. Alisema Godfrey

Pamoja na hayo Katibu huyo amefuta ile kauli yake aliyosema kuwa Nay wa Mitego na Prof Jay ndiyo wanaongoza kupeleka kazi zao kukaguliwa kabla ya kutoa na kusema alikuwa anawatolea mfano tu na laiti ingekuwa hivyo basi  msanii huyo angeshauriwa mapema kuwa wimbo huo haufai kutolewa kwa kukosa vigezo.

Aidha Katibu huyo amesema watamwita Nay wa Mitego ili kumpa nafasi ya kumsikiliza kwa upande wake ili aweze kusema ni kwanini ametoa wimbo wa aina hiyo.

Kwa upande mwingine Mngereza amesema wao na Jeshi la Polisi hawana uhusiano wowote kwa kuwa kila mtu anaongozwa na sheria zake alizokuwa nazo hivyo hata kukamatwa kwa msanii huyo amekamatwa kwa mujibu wa sheria za polisi na siyo BASATA.