Jumatano , 19th Jul , 2017

Msanii wa Bongo Fleva PNC amekanusha tuhuma za kukimbia mji na kuishi wilayani Mkuranga mkoani Pwani kwa lengo la kujificha asionekane baada ya watu kumwambia amefulia kimuziki. 

"Siyo kweli kwamba nilijificha Mkuranga, bali kule ni nyumbani kwetu. Watanzania wengi wanafikiria msanii akikaa kimya amefulia pasipo kujua wakati mwingine mtu anakuwa ameamua kutulia na kuna mambo mengine anayafanya" alisema msanii huyo alipozumza na eNewz ya EATV.

Hata hivyo msanii huyo amewataka watu kujua kukwama ni sehemu ya maisha na inaweza kumtokea mtu yoyote.

"Kukwama ni sehemu ya maisha inaweza kumtokea mtu yoyote. Mimi kuhusu kutoa nyimbo sikukwama kwani narekodi mara kwa mara ila video kidogo ndiyo nilikwama lakini nimerudi nitafanya kazi," alisema.

Hata hivyo PNC aliwahi kukaririwa akisema wasanii  wengi pamoja yeye wanakuwa wanashindwa kusonga mbele kwenye muziki kutokana na kukosa uongozi

 "Wasanii wengi tunayumba kutokana na kukosa uongozi mzuri, kwa sababu mimi naamini naweza kufanya kazi nzuri, natakiwa kupata uongozi ambao utaweza kusimamia kazi zangu nikaweza kupiga hatua kubwa zaidi kama watu wengine walivyoweza kupiga hatua , napata changamoto nyingi sana mimi siwezi kuusimamia muziki wangu wote nikaweza, nahitaji sapoti pamoja na ushauri", alisema PNC.