Ijumaa , 24th Mar , 2017

Msanii Timbulo ambaye kwa sasa anatamba na kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘mfuasi’ amesema hawezi kujiunga katika 'Label' ya QS Mhonda kwa kuwa hana imani nayo kama wanafanya biashara ya muziki.

Timbulo

Hayo yamekuja baada ya tetesi zilizoibuka kuwa msanii huyo amekataliwa kuingia katika uongozi wa Mhonda ambao ndiyo ulikuwa unasimamia kazi za Q Chillah hapo awali kabla hawajaingia katika vurumai ya kimkataba.

“Q Chillah ameshawahi kuwa na bendi  amefanya 'show' nyingi sana na watu wanajua hajawahi kufanya kitu chochote cha maajabu, kwa mimi binafsi sidhani kama QS ni menejementi ya muziki”. Alisema Timbulo wakati anahojiwa katika kipindi cha eNewz kutoka EATV.

Aidha msanii huyo amesema anamkubali sana Chillah ingawa kwa sasa siyo yule wa kipindi kile anayemfahamu katika ubora wake, huku akirusha kombora kwa Mhonda na kumwambia hajaona msaada aliyoutoa kwenye kuusogeza muziki wake (Chillah) zaidi ya msaada wa kimaisha ikiwemo kuwapa wasanii nyumba za kuishi na magari yakutembelea.

Kwa upande mwingine msanii huyo amesema ukimya wake katika muziki una faida kubwa kwani asingekuwa na usimamizi mzuri basi sasa hivi naye angekuwa katika kundi la kuutumia dawa za kulevya.