Jumatano , 19th Jul , 2017

Mwanamuziki anayefanya vizuri na ngoma yake mpya 'Kisela' ndani na nje ya nchi, Vanessa Mdee amefunguka na kusema kwamba hapendezwi na mapenzi ya kisela na kuwa yeye ni kiongozi wa kuyakemea mahusiano ya aina hiyo.

Vanessa ambaye hivi karibuni ameweka wazi kuachana na mpenzi wake Juma Jux amesema yeye na msanii huyo hawakuwa na mapenzi ya 'Kisela' bali walikuwa wana mapenzi ya dhati ingawa yameishia katikati.

"Mapenzi yangu na Juma hayakuwa ya Kisela, lakini pia sitaki na ninakemea kwa nguvu mapenzi ya kisela. Kuhusu kuimba wimbo huu nikwamba nimewasaidia wanawake wenzangu ambao huwa wanaingia kwenye mahusiano bila kujua ni mahusiano ya aina gani waliyonayo. Lakini kwenye uhalisia mimi siishi maisha hayo" - Vanessa .

Akizungumzia kuhusu kufanana sauti na mdogo wake ambaye ni msanii Mimi Mars, Vanessa amesema kwamba hana wasi wasi kufananishwa na ndugu yake huyo na kusema anaamini kila mmoja atatengeneza muziki mzuri na mashabiki wake.