Ijumaa , 27th Nov , 2020

Miamba ya soka Afrika vilabu vya Al Ahly na Zamalek vyote vya nchini misri vinataraji kukutana kwenye mchezo wa fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika mchezo unaotazamiwa kupigwa leo kwenye dimba la Cairo International nchini misri saa 4 kamili usiku kwa saa za Afrika ya mashariki.

Picha za mashabiki wa timu zote mbili

Mchezo huo unatazamiwa kuwa wakisasi kutokana na uhasimu wa kihistoria wa wawili hao kwenye ligi kuu misri na ubabe wa Al Ahly mbele ya Zamalek wa kuwafungwa kwenye michezo 5 na sare 3 Zamalek akiwa hajamfunga mpinzani wake huyo wa jadi kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika.

Kocha wa klabu ya Ahly Pitso Mosimane aliyejiunga na klabu hiyo mwezi septemba anapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo baada ya kuwahi kuwafunga Zamalek 3-1 mwaka 2016 na kutwaa kombe hilo akiifundisha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kabla ya kujiunga na Al Ahly.

Mosimane akifanikiwa kutwaa taji hilo basi atakuwa kocha watatu kwenye historia kuwahi kutwaa mataji hayo mara mbili akitwaa moja na klabu tofauti baada ya kulitwaa taji hilo mwaka 2016 mbele ya Zamalek.

Kwa Upande wa kocha wa Zamalek Mreno Jaime Pacheco amesema ana imani na ubora walionao wachezaji wake na kudai unaweza kuwafurahisha mashabiki zake kwa kufanya vizuri.

Mchezo huo unataraji kuingia kwenye vitabu vya historia kwa kuwa mchezo wa kwanza wa fainali ya michuano hiyo kuchezwa na vilabu viwili kutoka taifa moja, kuchezwa bila mashabiki na kuchezwa mchezo mmoja tokea mabadiliko ya kuacha kucheza michezo miwili ya fainali.

Mashabiki hawataruhusiwa kuingia uwanjani kuutazama mchezo huo kutokana na katazo lililotolewa na mamlaka ya afya na shirikisho la soka nchini misri kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa hatari wa korona unaoendelea kusumbua nchini misri na maeneo mengine dunia.

Ugonjwa wa Korona umeviathiri vilabu vya Al Ahlay na Zamalek ambao baadhi ya wachezaji na kocha msaidizi wamepatwa na ugonjwa wa korona siku chache zilizopita. Walid Soliman, Mahmoud 'Kahraba' Abdelmoneim na Saleh Gomaa ni wachezaji wa Al Ahly wenye COVI-19.

Kwa upande wa Zamalek, Mahmoud 'El Wensh' Hamdy na kocha wake msaidizi Medhat Abdelhady wameambukizwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

Mshindi wa kombe hilo anataraji kuweka kibindoni dola za kimarekani milioni moja sawa na bilioni mbili na milioni 319 za kitanzania wakati makamu bingwa akitaraji kupokea dola za kimarekani laki saba na nusu sawa na shilingi bilioni moja milioni mia saba thelathini na tisa.

Ikumbukwe kuwa, Al Ahly ndiye klabu bingwa kihistoria kwa kutwaa kombe hilo mara 8 wakati Zamalek wakibeba mara 5.