Jumatatu , 20th Feb , 2017

Kuelekea mchezo ujao wa watani wa jadi katika soka la Bongo, Simba na Yanga utakaopigwa Jumamosi ya tarehe 25/02/2017 katika dimba la Taifa Dar es Salaam, serikali imeonya mashabiki watakaofanya vurugu, huku askari 300 wakiwa wameandaliwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya serikali iliyotumwa kwa wanahabari na TFF, Serikali imesema kuwa kutakua na ulinzi wa kutosha ndani na nje ya Uwanja pamoja na kamera zenye uwezo wa kumuona kila mtu anayeingia Uwanjani na kila anachokifanya.

Kwa kutumia kamera hizo, serikali ambao ndiyo wamiliki wa uwanja huo watapiga picha na kuzirusha kwenye TV kubwa ya Uwanja kwa wale wote watakaobainika kuashiria/kutenda vurugu na sheria itachukua mkondo wake.

Imewataka wapenzi na mashabiki wa soka kuanza sasa kununu tiketi kwa njia wa kielektroniki ili kuondoa msongamano na lawama zisizo za lazima siku ya mechi

"Tunafahamu kuwa kuna changamoto za matumizi ya mfumo wa Ki- elektroniki lakini hatuna budi kuendelea kuelimishana na kujifunza kwani huko ndiko dunia ilipo,tutakua watu wa ajabu leo tukisema hatuwezi kutumia mfumo huu kisa changamoto hizi ndogondogo zinazojitokeza".

Hali ya uwanja baada ya vurugu za mechi ya Oktoba 01, 2016

Pia serikali imetoa rai kwa waamuzi waliopewa dhamana ya kuchezesha mchezo huu,wajue kuwa wana dhamana kubwa hivyo ni vyema wakafuata kanuni na sheria za mchezo husika ili kuepusha malalamiko.

Idara ya ulinzi ya TFF imesema imejipanga vilivyo ikiwa na askari takriban 300 kwa ajili ya kudhibiti fujo, huku bodi ya ligi ikisema waamuzi wa mchezo huo watafahamika siku chache zijazo.

Ikumbukwe kuwa mchezo uliopita wa timu hizi uliochezwa kwenye uwanja huu tarehe 1/10/2016 zilitokea vurumai zilizosababisha Serikali kuufungia Uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu. Vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo uvunjifu wa viti, mageti na mbaya zaidi baadhi ya watu walijerehuliwa.