Ijumaa , 18th Aug , 2017

Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC kupitia Afisa habari wao Jaffery Iddy Maganga amesema wameshamalizana na Kagera Sugar kuhusiana na sakata la Mbaraka Yusuph na sasa yupo huru kuitumikia Azam FC.

Maganga amebainisha hayo baada ya kuwepo mvutano wa muda mrefu kati ya Kagera Sugar na Azam FC ambapo kila timu ilikuwa inavutia upande wake, hatimaye mvutano huo umepata suluhisho.

"Jana tulifanya kikao na Kagera Sugar na mwisho tumefikia muafaka kuhusiana na suala hilo na sasa Mbaraka ni mchezaji halali wa Azam FC. Lakini bado hatujaanza kumtumia kwa sababu aliumia akiwa na timu ya Taifa hivyo bado yupo chini ya uangalizi wa daktari na anafanya mazoezi mepesi mepesi ili baadaye aweze kujiunga na kikosi kwa ajili ya mechi za Ligi" alisema Maganga.

Mshambuliaji Mbaraka Yusuph.

Pamoja na hayo, Maganga amesema timu ya Kagera Sugar  wametoa barua maalum ya kumuachia Mbaraka aitumikie Azam FC kwa sasa.

Mbaraka Yusuph amesaini kandarasi ya miaka miwili kuwatumikia wanarambaramba hao wa Vingunguti.