Alhamisi , 4th Mar , 2021

Klabu ya soka ya FC Barcelona imetinga fainali ya michuano ya kombe la mfalme (Copa del rey), baada ya kuifunga Sevilla mabao 3-0 kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali kwa ushindi wa jumla wa magoli 3-2.

FC Barcelona

Ushindi wa magoli 3-0 uliwafanya Barcelona kupindua matokeo baada ya kupoteza mchezo wa mkondo kwa bao 2-0. Mchezo huo ulichezwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kumalizika kwa Barcelona kuongoza 2-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 2-2 na hivyo dakika 30 zikaongezwa ili kumpata mshindi wa jumla.

Mabao ya ushindi ya Barcelona katika mchezo huo ambao ulipigwa katika dimba la Camp Nou yalifungwa na Ousmane Dembele dakika ya 12, Gerard Pique dakika ya 90 na Martin Braithwaite dakika ya 95. Mchezo huu pia ulishuhudiwa na wagombea wa Urais wa klabu hiyo wote watatu Joan Laporta, Toni Freixa na Victor Font.

Barcelona wamefuzu kucheza fainali ya mashindano haya kwa mara ya 42 na wakiwa wanauwinda ubingwa wa 31 na mpaka sasa ndio wanashikiria rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hii mara nyingi zaidi, wakiwa wametwaa ubingwa wa michuano hii mara 30.

Barcelona sasa watakutana na mshindi wa jumla wa mchezo wa nusu fainali ya pili kati ya Levante na Athletic Bilbao.