Jumatatu , 14th Aug , 2017

Beki mpya wa klabu ya Yanga, Gadiel Michael amesema atahakikisha anawazima washambuliaji wa timu ya Simba Agosti 23 mwaka huu John Boko, Laudit Mavugo pamoja na Emmanuel Okwi watakapokutana katika mechi yao ya Ngao ya Jamii hivi karibuni

Beki mpya Yanga, Gadiel Michael.

Beki huyo wa kushoto ambaye amejiunga na Yanga kwa kandarasi ya miaka miwili akiwa anatokea Azam FC amesema kwa upande wake mchezo huo utakuwa ni wa kawaida na amejipanga kuwadhibiti wachezaji hao watakaocheza kwenye eneo lake hadi kusahauliwa na mashabiki wa timu yao.

"Nadhani hiyo ndiyo mechi ambayo nitajitambulisha rasmi Yanga maana katika kucheza kwangu mpira, sijawahi kuogopa mechi kubwa hata siku moja wala kuwahofia wachezaji, na hao ambao watakuwa wanafika kwenye eneo langu wajue kabisa nitawazima kabisa siku hiyo. Naamini Mungu ataniongoza kwa kila kitu katika maisha yangu mapya", alisema Gadiel.

Kwa upande mwingine, timu ya Yanga jana imefanikiwa kuwanyoosha timu ya Mlandege bao 2-0 katika mechi yao ya kirafiki iliyochezewa mjini Zanzibar katika hatua ya maandalizi kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Tanzania Bara 2017/2018.