Jumapili , 13th Aug , 2017

Beki kisiki wa kati na nahodha wa timu ya Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema kujifunga kwa beki mpya wa timu hiyo hapo jana Abdallah Hajji ‘Ninja’  ni moja ya matukio ya mchezo na isitafsriwe kwamba beki huyo ni uchochoro au ana uwezo mdogo.

Cannavaro amesema 'Ninja' ni beki chipukizi mwenye uwezo mkubwa na kinachomkumba sasa hivi ni presha ya timu hiyo kutokana na kwanza ndiyo amesajiliwa na hakuwahi kucheza timu kubwa kama Yanga hivyo ana mambo ya kujifunza kwa wakati huu inabidi apewe muda ili azoee mazingira na baadaye matunda yake yataonekana.

Beki Hajji ‘Ninja aliyejifunga 

Cannavaro amesema hayo ikiwa ni siku moja tangu timu hiyo hapo jana jioni ipoteze mchezo wa kirafiki baada ya kufungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ambapo beki Hajji ‘Ninja’ alimfunga kwa kichwa cha mkizi kipa wake, Ramadhan Awam Kabwili dakika ya 22 wakati akijaribu kuokoa krosi ya Shalla Juma kutoka upande wa kushoto wa Uwanja na kuipatia bao pekee la ushindi Ruvu Shooting.

Huo ulikuwa mchezo wa pili wa kujipima nguvu kwa Yanga inayofundishwa na kocha Mzambia, George Lwandamina baada ya Jumamosi iliyopita kushinda 3-2 dhidi yas Singida United Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Na baada ya matokeo hayo, Yanga SC imeondoka hii leo jijini Dar es Salaam mapema kwenda Zanzibar ambako usiku huu watamenyana na Mlandege Uwanja wa Amaan katika mchezo mwingine wa kirafiki.

Mapema kesho Jumatatu Yanga watakwenda kisiwani Pemba kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba Agosti 23 Uwanja wa Taifa.