Jumamosi , 22nd Nov , 2014

Kufuatia bara la Afrika kukumbwa na janga la ugonjwa wa Ebola ambao umesababisha vifo kwa maelfu ya watu barani humu hasa kwa nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo shirikisho la kimataifa la mchezo wa Rollball duniani limesogeza mbele mashindano

Michuano ya mchezo wa rollball kwa nchini za Afrika na Asia AFRO-ASIAN Championships iliyokuwa ifanyike jijini kampala mwishoni mwa mwezi huu imeahirishwa mpaka mwakani mwezi wa nne baada ya timu za kutoka bara la Asia kuhofia ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa umeshika kasi kubwa katika baadhi ya mataifa barani Afrika

Mashindano hayo yalipangwa kupigwa jijini Kampala Uganda kuanzia Novemba 28 mwaka huu na hivyo sasa yatafanyika mwezi wa Nne katika mji huo huo wa Kampala lakini safari hii zikishiriki nchi za Afrika pekee

Mjumbe wa chama cha rollball Tanzania ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya rollball ya Tanzania Feruzi Juma ameiambia muhtasari wa michezo kuwa pamoja na hali hiyo wao bado wanaendelea kujiandaa na mashindano yoyote yatakayojitokeza mbele yao na bahati pekee katika kipindi hiki ambacho mashindano hayo yamesogezwa mbele timu yao imepata mwaliko wa kucheza mchezo mmoja na wenzao wa Kenya mchezo ambao utafanyika kati ya mji wa Arusha au Nairobi mapema mwezi ujao

Feruzi ametumia fulsa hiyo kuwashukuru wadhamini na wadau mbalimbali waliojitokeza kutoa misaada yao hasa suala la nauli na vifaa ambavyo watavitumia katika mashindano mbalimbali lakini pia bado wanakaribisha misaada zaidi katika nyanja mbalimbali ili wajiandae vema na hatimaye wakafanye vizuri katika michuano hiyo.