Jumanne , 26th Oct , 2021

Kocha wa zamani wa Inter Milan, Antonio Conte huenda akatwaa mikoba ya Kocha wa sasa wa Manchester United Ole Gunnar Soljsker, ambaye amekuwa na muenendo mbaya wa matokeo ndani ya hiyo ya mashetani wekundu.

Antonio Conte

Conte mwenye sifa na asili ya ushindi kwenye timu zote alizofundisha, alifurahia maisha bora ya uchezaji, ambapo mafanikio mengi aliyapata akiwa na Juventus na umaarufu katika klabu ya Lecce, timu ya nyumbani kwao lakini akasajiliwa na Giovanni Trapattoni na kuhamia Turin mwaka wa 1991.

Mataji matano ya Serie A yalifuata, na mafanikio mengine yakija kupitia Coppa Italia, Supercoppa Italiana, UEFA Cup, UEFA Super Cup na UEFA Intertoto Cup.

Pia alishinda UEFA Champions League mwaka wa 1995/96 akiwa mchezaji na kumaliza kama mshindi wa pili katika mashindano hayo mara nyingine tatu.

Conte, ambaye aliwakilisha Italia kwenye Kombe la Dunia mwaka 1994 na mashindano ya UEFA ya 2000, alitundika daruga mnamo mwaka 2004 na kugeukia ukocha.

Baada ya kuanza kama kocha msaidizi wa Arezzo mnamo 2005/06, alikabidhiwa jukumu lake la kwanza la usimamizi na klabu hiyo Julai 2006, kabla ya kuhamia Bari mnamo Desemba 2007.

Katika msimu wake wa kwanza kamili wa kufundisha, Bari walitawazwa mabingwa wa Serie B na kupandishwa daraja hadi Serie A kwa msimu wa 2009/10.

Alifundisha katika vipindi vifupi akiwa na Atalanta na baadaye kuiongoza Siena kurejea ligi kuu ya Italia, na kufanikiwa kumpa Conte nafasi ya kuhamia Juventus Mei 2011.

Mataji matatu mfululizo ya Serie A alishinda chini ya usimamizi wake, pamoja na mafanikio ya mfululizo ya Supercoppa Italiana 2012 and 2013.

Akifurahia matunda ya mafanikio hayo Turin, ambapo alishinda Panchina d'Oro - tuzo ya kocha bora wa Serie A wa msimu kwanzia mwaka 2012 mpaka 2014.

Baada ya kujiuzulu majira ya joto ya 2014, Conte alichukua nafasi ya Cesare Prandelli kama kocha mkuu wa Italia, akiiongoza Azzurri kufika hatua ya robo fainali UEFA Euro 2016.

Kufuatia kushindwa kwa Italia katika robo fainali ya UEFA Euro 2016 na Ujerumani, Conte alijiunga na Chelsea kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na kuwaongoza The Blues, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza 2016/17.

Alishinda taji hilo katika jaribio la kwanza, huku pia akiwapeleka Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA, ambapo walipoteza kwa Arsenal msimu huo.

Conte alirekebisha kipigo hicho kwa kushinda kombe mwaka mmoja baadaye katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Manchester United lakini The Blues ilitangaza kuwa wameachana na kocha huyo tarehe 13 Julai 2018.

Raia huyo wa Italia alikaa nje ya soka kwa mwaka mmoja na mpaka Mei 2019, Antonio Conte alifanywa kuwa kocha mkuu wa Inter Milan, na chini ya uongozi wake, Inter Milan ilimaliza utawala wa Juventus wa miaka 10 kwenye ubingwa wa Serie A.

Kufuatia kile ambacho kingekuwa msimu mzuri baada ya ushindi huo, Conte alijiuzulu baada ya klabu hiyo kusema kuwa itawauza wachezaji ili kupunguza gharama ya mishahara.