Jumapili , 15th Oct , 2017

Bingwa wa Wimbledon Roger Federer ametwaa ubingwa wa Shanghai Masters baada ya kumfunga mchezaji namba moja duniani kwa ubora Rafael Nadal seti 6-4 6-3 katika fainali iliyomalizika mchana huu.

Federer raia wa Uswis ametwaa taji lake la sita ndani ya mwaka 2017, akiwa ndiye mchezaji pekee aliyemshinda Nadal mara nne ndani ya mwaka huu.

Mswis huyo mwenye umri wa miaka 36, alikuwa kwenye kiwango kizuri leo baada ya kumlaza Nadal kwa muda wa dakika 72 pekee.

Federer sasa ndio mchezaji pekee ambaye anaweza kuchukua nafasi ya Nadal kama mchezaji namba moja duniani mwishoni mwa mwaka huu, lakini michuano ya ATP kwenye uwanja wa London 02 mwezi ujao ndio itaamua.

Kwa upande wa wanawake Maria Sharapova ameshinda taji la kwanza tangu Mei 2015, baada ya kumpiga Aryna Sabalenka 7-5 7-6 10-8 katika fainali ya Wazi ya Tianjin mchana wa leo.