Jumanne , 14th Nov , 2017

Mchezaji tenisi namba moja duniani Rafael Nadal amemaliza vibaya msimu baada ya kutupwa nje ya fainali za dunia za ATP zinazoendelea jijini London Uingereza.

Mhispania huyo ameondolewa kwa kipigo cha seti 7-6 (7-5) 6-7 (4-7) 6-4 kutoka kwa David Goffin. Katika mchezo huo uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwenye uwanja wa 02 jijini London, Nadal alilazimika kucheza huku akiwa na maumivu ya goti.

Nadal aliumia goti kwenye mchezo wa robo fainali ya michuano ya Paris Masters wiki iliyopita hivyo akalazimika kujitoa ili aweze kutibiwa haraka akipigania kurejea mapema kucheza fainali za kufunga msimu huu za ATP jijini London.

Hata hivyo imekuwa ngumu kwa nyota huyo kuendelea na mashindano kutokana na kipigo hicho cha mechi yake ya ufunguzi kutoka kwa David Goffin ambaye ni raia wa Ubelgiji. Nadal amesisitiza kuwa hata kama angeshinda ilikuwa lazima ajitoe kutokana na kushindwa kuhimili maumivu ya goti.

Kuondolewa kwa Nadal kunatoa fursa kwa mkongwe Roger Federer kuisaka nafasi ya kuwa bingwa wa fainali hizo. Pamoja na kutolewa kwake lakini Nadal tayari ameshajihakikishia kumaliza msimu huu akiwa mchezaji namba moja duniani hata kama mpinzani wake mkubwa Roger Federer atatwaa ubingwa wa ATP.