Alhamisi , 15th Apr , 2021

Kocha wa Manchester City,Pep Guardiola amemvulia kofia kiungo kinda wa klabu ya Borrusia Dortmund, Jude Bellingham mwenye umri wa miaka 17 kwa kuonesha uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu ilhali akiwa na umri mdogo tena kwenye michuano ya klabu bingwa barani Ulaya usiku wa jana April 14, 2021

Pep Guardiola (kushoto) na Jude Bellingham (kulia).

Guardiola ameyasema hayo baada ya mchezo wa timu yake ya Manchester City kuifunga Dortmund mabao 2-1 ugenini kwenye uwanja wa Signal Iduna park nchini Ujerumani na kufuzu hatua ya nusu fainali kwa jumla ya mabao 4-2 baada ushindi wa maba0 2-1 kwenye mchezo wa kwanza.

Pep amesema, “Siwezi kuamini,huenda ni muongo! Yupo vizuri sana kama hana umri wa miaka 17, ni mchezaji bora sana. Kuna muda hakupasiwa mpira kutoka kwa walinzi wa kati wa timu yake, namna alivyoongea kwa kufoka na kutaka apasiwe yeye kwa umri alionao ina maan akubwa sana”.

“Niliongea na kocha wake, Edin Terzic, na aliniambia unachokiona sasa ndicho anachofanya kila siku akiwa mazoezini”.

(Jude Bellingham akishangilia baada ya kufunga bao dhidi ya Manchester City usiku wa jana.)

Bellingham baada ya kuonesha soka safi na kufunga bao la kufutia machozi ameweka rekodi kadhaa, amekuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mdogo miaka 17 na siku 289 kufunga bao kwenye michuano hiyo akiwa raia wa England na kuwapiku, Theo Walcott na Oxlade Chamberlin.

Na bao lake hilo, ndilo bao lake la kwanza kwenye michuano hiyo, na la kwanza akiwa na Dortmund kwenye michuano hiyo tokea ajiunge nao mwezi wa saba mwaka 2020.

Jude Bellingham amecheza michezo 39 kwenye michuano yote, akifunga mabao 3 na kutengeneza mabao 4.