Jumatatu , 30th Nov , 2020

Kocha wa Tottenham Jose Mourinho, ameitoa timu yake kwenye mbio za ubingwa wa ligi kuu nchini England, licha ya kuwa vinara wa ligi hiyo na amekifananisha kikosi chake na Farasi mdogo kwenye mbio za kuwania ubingwa.

Kocha wa Tottenham Jose Mourinho, ameitoa timu yake kwenye mbio za ubingwa wa EPL licha ya kuwa ninara wa ligi hiyo

Tottenham wamerejea tena usukani mwa msimamo wa EPL, baada ya kupata suluhu dhidi ya Chelsea kwenye mchezo wa ligi katika dimba la Stanford Bridge jana usiku, na suluhu hiyo imeifanya Tottenhama kufikisha alama 21 sawa na mabingwa watetezi Liverpool walio nafasi ya pili wakati Chelsea wapo nafasi ya 3 wakiwa na alama 19.

Licha ya kuianza wiki ya pili mfululizo wakiwa wanaongoza lakini Jose Mourinho alipoulizwa kuhusu kikosi chake kuwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu alijibu,

“Hatuko hata kwenye mbio kwa hivyo sisi sio farasi. Sisi ni farasi mdogo, mchanga. unaona tofauti” Mourinho aliwaambia wanahabari.

Spurs wamepoteza mchezo 1 tu kwenye michezo 10 ya ligi waliyocheza mpaka hivi sasa, na wamekusanya alama 13 kwenye michezo yao 5 ya mwisho ukiwa ni wasitani mzuri wa kupata alama kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 1992-93.

Kwa upande mwingine Mourinho pia amesisitiza Chelsea ipo kwenye nafasi ya kutwaa ubingwa ukilinganisha na kikosi chake.

“Wao ni moja ya washindani wakubwa, hakuna shaka juu ya hilo, ninaamini kwamba kwao sio shida hata kidogo kuwa nyuma ya Liverpool kwa alama mbili, nadhani.

Wanajua jinsi wana nguvu na kikosi walicho nacho. Na wanajua kuwa huu ni msimu mrefu. Pia wanajua kuwa Tottenham sio washindani”.

Hii sio mara ya kwanza Jose Mourinho kuiondoa timu anayoifundisha kwenye mbio za ubingwa kwani hata msimu wa 2014-15 akiwa na kikosi cha Chelsea alikifananisha kikosi hicho na Farasi mdogo kwenye mbio za ubingwa na mwishoni mwa msimu wakatwaa ubingwa.

Mchezo wa ligi unaofata Tottenham watawaarika majirani zao kutoka London Kaskazini Arsenal Disemba 6.