Ijumaa , 20th Oct , 2017

Klabu ya soka ya Kagera Sugar imeendelea kupigana kusaka ushindi wa kwanza kwenye ligi kuu ya soka Tanzania Bara baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Mwadui FC jioni ya leo.

Katika mchezo huo Kagera imeponea chupuchupu kupoteza mechi hiyo baada ya kuwa nyuma kwa bao moja lililofungwa mapema dakika ya 10 na mshambuliaji wa zamani wa Yanga Paul Nonga.

Baada ya mapumziko kikosi cha Meck Mexime kilionekana kuwa na kiu ya kusawazisha na kuongeza bao ili kuchukua alama tatu za kwanza lakini ikashindikana na mwisho dakika ya 87 Jaffary Kibaya akaipatia bao la kusawazisha timu yake, hivyo kuiwezesha kupata alama moja.

Kagera inaendelea kuburuza mikia ikiwa na alama 3 baada ya michezo 7 huku Mwadui ikisogea hadi nafasi ya 11 kutoka 12 ikisubiri matokeo ya kesho ambapo Njombe Mji iliyorudi nafasi ya 12 itakuwa uwanjani dhidi ya Simba SC.

Ligi kuu ya VPL itaendelea kesho kwa jumla ya mechi sita za raundi ya 7 kuchezwa kwenye viwanja tofauti. Azam FC watakuwa wageni wa Mbao FC jijini Mwanza wakati Simba wataialika Njombe Mji.