Jumatatu , 23rd Oct , 2017

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara VPL timu ya Yanga inatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam siku ya Jumanne ikitokea Shinyanga ambako jana ilicheza mchezo wa raundi ya saba dhidi ya Stand United.

Hilo limethibitishwa na msemaji wa Yanga Dismas Ten ambaye emeeleza kuwa timu itaanza safari ya kutoka Shinyanga kurejea Dar es salaam siku ya Jumanne Oktoba 24.

“Timu inatarajiwa kurejea jijini Dar es salaam siku ya kesho Jumanne Oktoba 24 mwaka huu ambapo itapumzika na kisha taratibu zingine za maandalizi ya mchezo wa Oktoba 28 dhidi ya Simba zitaendelea”, amesema Ten.

Hata hivyo msemaji huyo hajafafanua ni wapi timu hiyo itaweka kambi kwaajili ya maandalizi hayo huku kukiwa na tetesi kwamba huenda ikaweka kambi nje ya Dar es salaam japo bado haijabainika ni wapi haswa.

Yanga jana iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya wenyeji Stand United kwenye uwanja wa CCM Kambarage na kufanya ifungane pointi na vinara Simba ambayo nayo ilishinda mechi yake dhidi ya Njombe kwa mabao 4-0 hali inayosababisha kuongezeka kwa ushindani kwenye mchezo wao wa Jumamosi.