Jumatano , 14th Jun , 2017

Beki mpya wa Mabingwa wa kombe la Shirikisho (FA) Simba SC, Shomari Kapombe amefunguka kwa kudai timu yake hiyo itakuwa tishio katika msimu ujao kutokana na usajili unaofanywa na klabu hiyo.

Shomari Kapombe

Kapombe amesema hayo baada ya kuona jitihada za uongozi wake mpya zikiwa zinalenga kuimarisha kikosi chake kwa kuwachukua wachezaji waliofanya vizuri katika msimu ulioisha hivi karibuni.

“Ukiangalia usajili unaofanyika sasa na kikosi kilichopo, hakuna ubishi kwamba Simba itakuwa na kikosi kizuri, maana yake ni kwamba, tuna nafasi ya kufanya vizuri na litakalofuata ni maandalizi mazuri na ushirikiano wa kutosha" alisema Kapombe ambaye amerejea Simba.

Kapombe amekuwa mchezaji wa tano kusajiliwa Simba SC na watatu kutoka timu ya Azam FC msimu huu baada ya kusajiliwa John Bocco na Aishi Manula huku beki Yusuf Mlipili toka Toto Africans na Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC.