Jumatatu , 30th Nov , 2020

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 20 'Ngorongoro Heroes' inatazamiwa kujitupa dimbani hii leo kucheza dhidi ya timu ya taifa ya vijana ya Sudan Kusini mishale ya saa tisa na nusu alasiri kwenye dimba la Black Rhino, karatu jijini Arusha.

Vijana wa Ngorongoro Heroes wakiwa katika matayarisho ya michezo yao ya Cecafa.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha wa Ngorongoro Heroes, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na hali za wachezaji wake ni nzuri na tayari kuwavaa wapinzani wao nakusisitiza lengo ni kupata ushindi na kushiriki AFCON ya vijana mwaka ujao.

Kwa Upande wa mwingine, Mchezaji wa Ngorongoro Heroes Mlinzi wa kulia David Kameta amesema wapo vizuri kisaikolojia na kubwa ni watanzania waungane pamoja kuwaaombea ili waweze kuwafurahisha kwa kupata ushindi hii leo na kutinga fainali na hatimaye kuwa mabingwa.

Ngorongoro Heroes inapigiwa chepuo na wafuatiliaji wengi wa soka nchini huenda ikabeba ubingwa huo kufuatia kiwango safi ambacho wamekionesha hatua ya makundi kwa kuwafunga Djibout 6-1 na kuwashushia zahma Somalia kwa kuwafunga 8-1 na kutinga nusu fainali.

Mchezo wa nusu fainali ya kwanza ni ule utakaowakutanisha timu ya taifa ya vijana ya Uganda dhidi ya Kenya mchezo unaotazamiwa kuchezwa saa 6 kamili mchana kwenye dimba la Black Rhino, Karatu jijini Arusha.

Washindi wa nusu fainali hizo wanataraji kukutana kwenye fainali 2 Disemba 2020.