Jumatatu , 22nd Mei , 2017

Safari ya Serengeti Boys - timu ya Tanzania ya Vijana wenye umri wa miaka 17, inaendelea licha ya jana Mei 21, mwaka huu kuondolewa kwenye hatua ya makundi ya kuwania taji la Afrika hapa Port Gentil nchini Gabon.

Wachezaji wa Serengeti Boys wakiwa nchini Gabon

Akizungumzia matokeo hayo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema: "Kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi."

Alizungumza hayo kwa nyakati tofauti, Malinzi alisema: "Tujipange sasa kwa yafuatayo: Michezo ya kufuzu (Qualifiers za 2019 Afcon U20  zinafanyika mwakani kuanzia mwezi June. Vijana hawa watashiriki.

"AFCON U17 finals (Fainali za AFCON za vijana wenye umri wa chini ya miaka 17) zinafanyika Tanzania mwaka 2019," amesema Malinzi na kuongeza: "Serengeti Boys hii ya sasa inakuwa Ngorongoro Heroes (Vijana wa u20 na ikishapumzika kwa muda, itaingia tena kambini."

Amesema kwamba vijana wa Tazania wenye umri wa chini ya miaka 15, walioko Shule za Alliance Mwanza wanakuwa Serengeti Boys wapya.

"Hakuna muda wa kusononeka ni kuchapa kazi tu. Kikubwa tunaandaa Taifa Stars ya kwenda World cup 2026 na qualifiers zake zitaanza mwaka 2024. Kwa sasa timu inajiandaa kuingia kambini kwa ajili ya kuivaa Lesotho," amesema.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime amesema timu yake imepoteza mchezo huo kwa makosa ya kimchezo na bahati haikuangiwa kwa vijana wa Tanzania katika mchezo dhidi ya Niger.

Serengeti Boys ilifungwa bao 1-0 na Niger katika mchezo uliofanyika , hivyo kufanya matokeo ya timu zote mbili kufanana kwa pointi, idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa tangu kuanza kwa fainali hizi za AFCON, Mei 15, mwaka huu.