Jumapili , 15th Jan , 2017

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amemkubali na kumnyooshea mikono kocha msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche kwa kukibadilisha kikosi chake na kukifanya kiwe cha ushindani.

Haji Manara (Juu), Cheche (Chini)

Manara amesema Cheche ameonesha uwezo mkubwa kwani kabla hajakabidhiwa timu hiyo, kikosi cha Azam kilikuwa dhaifu kiasi cha kutopewa hata nafasi kwenye michuano ya Mapinduzi iliyomalizika juzi na kushuhudia ikiondoka na ubingwa.

Azam iliifunga Simba bao 1-0 katika mchezo wa fainali wa michuano hiyo huku ikionesha kandada safi na kumaliza michuano hiyo bila kufungwa bao hata moja

"Kwa kweli Azam imebadilika sana, nampongeza sana kocha Cheche, amefanya kazi kubwa ndani muda mfupi kikosi kimebadilika sana, inaonekana sasa wachezaji wanamuelewa kocha, na kazi aliyoifanya kwenye Mapinduzi siyo ndogo, timu imeweza kumaliza mechi tano bila kufungwa bao hata moja, siyo jambao dogo" Alisema Manara

Cheche alikabidhiwa mikoba ya kikosi hicho mara baada ya kufungashiwa virago kwa aliyekuwa kocha mkuu Zeben Hernandez na wasaidizi wake wote mara baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.

Hivi sasa Cheche atafanya kazi kama kocha msaidizi mara baada ya Azam kupata kocha mkuu raia wa Romania.