Jumamosi , 20th Mei , 2017

Timu ya Mbao FC ya Mwanza leo imefanya maajabu kwa kufanikiwa kubaki ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwachapa mabingwa wapya wa ligi hiyo, Yanga SC bao 1-0 katika mchezo uliopigwa dimba la CCM Kirumba Mwanza.

Kikosi cha Mbao FC

Hii inaweza kuwa ni maajabu kutokana na ukweli kuwa Yanga ndiyo mabingwa wa ligi hiyo na Mbao ni timu ambayo ilipanda daraja kupitia mlango wa nyuma ikiwa haina matayarisho yoyote baada timu 3 kushushwa daraja katika kundi lao baada ya ligi daraja la kwanza msimu uliopita wa 2015/16.

Katika mchezo wa leo ambao ulikuwa ni moja kati ya michezo 8 ya kufunga pazia la ligi hiyo, Mbao ilianza kipindi cha kwanza kwa kasi ya ajabu na kufanikiwa kupata bao hilo dakika ya 23 kupitia kwa Haji, likiambatana na kosa kosa kadhaa katika kipindi hicho cha kwanza.

Mbao iliyotawala zaidi kipindi hicho haikuipa kabisa Yanga mwanya kubadili ubao wa mabao na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Mbao ilikuwa na umiliki wa asilimia 55 dhidi ya 45 za Yanga.

Kwa matokeo haya Mbao imefanikiwa kufikisha pointi 33 huku ikiziacha African Lyon ikiwa na pointi 32, Toto African yenye pointi 29 na JKT Ruvu ikiwa mkiani na pointi 23 timu ambazo zimeungana kushuka daraja rasmi.

Walioshuka daraja

Toto wamefungwa na Mtibwa Sugar mabao 3-1 huku African Lyon ikilazimishwa sare na Tanzania Prisons. Timu nyingine iliyonusurika leo ni Ndanda FC ambayo imeifunga JKT Ruvu mabao 2-0.

Yanga imetwaa rasmi ubingwa wa ligi hiyo ikiwa na pointi 68 sawa na Simba lakini ikiipiku Simba kwa idadi ya magoli na leo katika dimba la CCM imekabidhiwa kombe lake, ukiwa ni ubingwa wa 3 mfululizo.

Ubingwa huo huenda 'ukatumbukia nyongo' kutokana na rufaa ya Simba ambayo wameikata FIFA wakidai kupewa pointi 3 kutokana na mchezo wake dhidi ya Kagera, ambapo wanadai Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji asiyestahili.

Nafasi ya tatu imekwenda kwa Kagera Sugar ambayo leo imeichapa Azam FC bao 1-0 katika dimba la Chamazi na kufikisha point 53 nyuma ya Simba na Azam ikibaki na pointi 52 katika nafasi ya 4. Mtibwa Sugar imekamata nafasi ya 5 ikiwa na pointi 44.

Stand United imemaliza katika nafasi ya 6 ikiwa na pointi 38, ikifuatiwa na Ruvu Shooting nafasi ya 7 na pointi 36, Majimaji nafasi ya 8 na pointi 35, Tanzania Prisons nafasi ya 9 na pointi 35, Mwadui pointi 35 na Mbeya City point 33.